Taarifa kwa wanachama kuhusu magari yaliyokamatwa Zambia

Ndugu wanachama tumepata taarifa ya magari zaidi ya 200 ya baadhi ya wanachama wetu kushikiliwa na mamlaka ya serikali ya Zambia katika maeneo mbalimbali inchini humo. Inasemekana magari hayo yalikuwa yamebeba magogo ya Mbao kutoka nchi ya Kongo na Mengine kutoka Zambia.

Kama mnavyofahamu serikali ya Zambia ilishapiga marurufuku usafirishaji kwenda nje wa magogo yote ya mbao, hivyo basi mamlaka ya nchi hiyo inahisi kuna udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wakishirikiana na watumishi wasiokuwa waaminifu kusafirisha magogo ya nchi hiyo kwa kutumia vibali vya nchi ya Kongo. Hii imepelekea magari yote yaliyokuwa yamebeba mzigo huo kwa nia ya kuusafirisha kupitia bandari yetu kuzuiwa.

Uongozi wa TATOA unafanya juhudi za kuwasiliana na Mamlaka za Zambia kupitia Wizara ya mambo ya nchi za nje ili kuiomba serikali ya Zambia ifanye uchunguzi wa haraka wa kubaini magari yaliyopakia magogo ya nchi ya Kongo na yale yanayosemekana kupakiliwa magogo ya Zambia kwa kutumia nyaraka za udanganyifu kutoka Kongo.

Uchunguzi wa haraka utasaidia kubaini mzigo na nyaraka zilizofanyiwa udanganyifu na wahusika kuchukuliwa hatua stahiki na mzigo usiokuwa na tatizo uweze kuruhusiwa ili kupunguza hasara kubwa wanayoendelea kuipata wanachama vilevile hatua za haraka zitasaidia kuondoa usumbufu kwa madereva ambao wanaendelea kuteseka kutokana na kadhia hiyo.

Tunaomba wale wote walioguswa na tatizo hili wawasiliane na uongozi haraka kwani mpaka sasa tumepokea orodha ya magari 60 tu kati ya magari yanayosemekana kufikia 200.

Tunatoa rai kwa wanachama wetu kijiepusha kwa namna yoyote kupakia mizigo isiyokuwa na nyaraka timilifu au ambayo imepigwa marufuku kusafirishwa na mamlaka za nchi mbalimbali pamoja na ile ambayo haijalipiwa kodi. Hakikisheni mnazisoma nyaraka zote kabla ya kupakia mzigo na kuhakiki kama zina vibali vyote vinavyotakiwa ikiwemo risiti za EFD kwa mzigo wa ndani.

“umoja ndio Mafanikio yetu”

Mwenyekiti Bodi ya Wakurugenzi – TATOA
Dar Es Salaam 31-03-2017

No Comments

Post a Comment