Njia 5 teknolojia inaweza kuisaidia biashara yako ya usafirishaji 2017

Katika miaka ya hivi karibuni,teknolojia imekuwa ikiongezeka kwa kasi kubwa duniani kote na kusababisha sekta mbalimbali kubadilisha mbinu zao za kufanya biashara. Sekta ya usafirishaji hasa katika bara la Afrika, kwa sehemu kubwa ilikuwa haijaguswa na mabadiliko haya ya kiteknolojia duniani; lakini kutokana na kuongezeka kwa gharama za kufanya biashara katika miaka ya hivi karibuni pamoja na kuongezeka kwa ushindani kwa ajili ya kazi, imekuwa ni muhimu kwa kampuni za usafirishaji kufanya kazi kwa ufanisi ili kuhakikisha faida kubwa. Ili kufikia malengo hayo, katika makala hii tutapitia teknolojia tano ambazo kama zikitumika kwa usahihi zinaweza kusaidia makampuni ya usafirishaji katika kufuatilia na kusimamia rasilimali zao.

1. Programu ya Usimamiaji wa Magari (Fleet Management Software )
Programu za usimamiaji wa magari zinasaidia kuhifadhi taarifa mbalimbali za magari, taarifa za madereva, taarifa za matengenezo ya magari pamoja na taarifa juu ya mizigo inayobebwa na magari na gharama za usafirishaji. Kama programu hizi zikitumika vizuri zinaweza kusaidia kuongeza ufanisi wa shughuli za usafirishaji kwa kusaidia kufuatilia na kusimamia gharama zinazotumika kwa kila safari ya gari; taarifa ambazo husaidia kampuni kupangilia vyema rasilimali zake ili kuondoa hasara, kuongeza faida na kuweka mipango bora ya baadaye kwa kuzingatia taarifa zilizokusanya na programu hizi, kama vile kiwango cha tairi kuisha, njia za usafirishaji zenye gharama nafuu zaidi, mahitaji ya mafuta ya gari kwa mwaka nk

2. Teknolojia ya kufuatilia magari (Tracking Software)
Teknolojia ya kufuatilia magari inaonekana ndio teknolojia iliyopokelewa kwa urahisi zaidi na makampuni mengi ya usafirishaji. Mfumo mzuri wa kufuatilia magari husaidia uongozi wa makampuni ya usafirishaji kusimamia kwa urahisi zaidi magari yaliyoko njiani yakisafirisha mizigo. Mifumo hii husaidia uongozi wa makampuni kuhakikisha kwamba madereva wao wanafuata maelekezo waliyopewa na wanafuata sera za kampuni kama mahali yanaporuhusiwa kuegesha magari, kutokuendesha mida ya usiku na kutokubeba mizigo isiyokuwa ya kiofisi.

3. Programu za usimamzi wa fedha (Accounting / Finance Software)
Programu za usimamizi wa fedha ni za umuhimu wa juu kwa biashara yoyote duniani lakini idadi kubwa ya makampuni bado hutumia kalamu na karatasi kurekodi taarifa zao za kiuhasibu. Programu za usimamizi wa fedha zipo za aina nyingi zilizotengenezwa kutumika na makampuni ya ukubwa tofauti kutoka yale madogo kabisa, hadi makubwa kabisa. Programu za uhasibu husaidia biashara kufuatilia mtiririko wa fedha zake, kama msemo wa Kiswahili unavyosema, “Mali bila daftari, hupotea bila Habari”. Tofauti na mbinu ya kutumia kalamu na karatasi, programu hizi husaidia makampuni kukusanya na kuhifadhi taarifa zao za fedha kwa ufanisi zaidi kwa kupunguza makosa ya kibinadamu huku yakirahisisha upatikanaji wa ripoti zinazosaidia kampuni kuweka mipango thabiti ya kukuza biasha yake.

4. Programu za Huduma kwa Wateja (Customer Relationship Management Software – CRM)
Programu za huduma kwa wateja (CRM) ni programu ngeni kwa makampuni mengi ya Afrika. Programu za huduma kwa wateja husaidia makampuni kuhifadhi vyema taarifa za wateja wao na kusaidia kufuatilia miongozo ya kupata wateja wapya. Programu hizi husaidia makampuni kutambua wateja wao wakubwa na pia tabia za wateja wao ili kusaidia makampuni kufanya maamuzi sahihi juu ya namna bora ya kuwahudumia wateja wao.

5. Mwonekano wa Mitandaoni (Online Presence )
Hili hasa limekuwa jambo gumu kwa makampuni mengi ya usafirishaji duniani kote kuzingatia kutokana na sekta hii kwa kiasi kikubwa kuendelea kutumia njia za kizamani za kufanya biashara. Katika zama hizi za mitandano ya kijamii na simu zenye uwezo mkubwa ‘smart phones’ mwonekano wa mitandaoni ni lazima kwa kampuni yoyote inayotaka kuleta ushindani. Mwonekano wa mitandaoni ina maana angalau kampuni inatakiwa iwe na tovuti yake yenye taarifa sahihi za kampuni pamoja na kurasa katika mitandao ya kijamii. Zana hizi za mitandaoni kama ikitumika ipasavyo itasaidia makampuni kupata wateja wapya na kurahisisha wateja wao wa zamani kupata taarifa za kampuni kwa urahisi zaidi.

No Comments

Post a Comment