Mtizamo wa TATOA juu ya kushuka kwa idadi ya mizigo bandari ya Dar-Es-Salaam

Katika miezi ya karibuni Tanzania imeshuhudia kushuka kwa kiasi kikubwa kwa kiwango cha mizigo inayopita bandari ya Dar es Salaam hususan mizigo inayopitishwa kwenda nchi za jirani. TATOA imechunguza na kutafakari sababu zinazosababisha kushuka huko kwa kiwango cha mizigo na imegundua sababu zifuatazo;

1. Kutotangazwa vizuri kwa bandari ya Dar-Es-Salaam na wahusika

Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikikabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa bandari za nchi jirani za Mombasa (Kenya), Beira (Msumbiji) na Durban (Afrika Kusini). Serikali za nchi hizo zimeendesha kampeni za kuzitangaza bandari zao katika nchi jirani zisizokuwa na bandari ili kuwashawishi wafanyabiashara wa huko kutumia bandari zao. Kwa upande wake, Tanzania haijawa na mikakati yoyote ya kutangaza bandari zetu katika nchi jirani. Hili limesababisha bandari zetu kukosa wateja wanaohamia bandari shindani kwenye nchi za jirani. Serikali ya Kenya kwa mfano hutumia asilimia kumi (10%) ya kipato chake kuitangaza bandari ya Mombasa.

2. Matatizo yanayoletwa na utekelezaji wa Himaya ya Umoja wa Forodha (Single Customs Territory) kwa mizigo ya DRC

Himaya ya Umoja wa Forodha na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ilianzishwa ili kuharakisha upitishwaji wa mizigo iliyokuwa inaelekea DRC kupitia bandari ya Dar es Salaam na kusaidia kuzuia ukwepaji wa kodi. Hata hivyo, utekelezwaji wa himaya hiyo ya forodha umekutana na matatizo mbalimbali yaliyosababisha kuongezeka kwa idadi ya siku mizigo ya DRC huchukua mpaka ipitishwe bandarini hadi kufikia miezi miwili au mitatu.

Zaidi ya hayo, wafanyabiashara wa Kongo, kupitia himaya hii ya forodha hivi sasa wanahitajika kulipa kodi zote za nchini mwao hapa hapa Tanzania. Hili limesababisha baadhi ya wafanyabiashara wa Kongo kupendelea kupitisha mizigo yao katika nchi nyingine zisizokuwa na makubaliano ya himaya ya umoja wa forodha na serikali yao.

3. Suala la kutoza VAT kwa usafirishaji wa mizigo ya transit

Hili ni suala ambalo TATOA imekuwa ikilisemea mara kwa mara kwa taasisi husika za Serikali. Kulingana na sheria mpya ya kodi ya mwaka 2015, kampuni za usafirishaji zinatakiwa kulipa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye shughuli za usafirishaji, hata pale inaposafirisha mizigo inayoelekea nje ya nchi (transit cargo). Jambo hili linachangia kuongezeka kwa gharama za kufanya biashara kwa wasafirishaji wa Tanzania ambayo pia inasababisha kuongezeka kwa gharama za usafirishaji wateja wanayotozwa. Hili limesababisha baadhi ya wafanyabiashara kupitishia mizigo yao kwenye bandari za nchi ambazo gharama za usafirishaji wa bidhaa hizo uko chini.

4. Taarifa mbaya za bandari ya Dar-Es-Salaam kufikia nchi za jirani

Hivi karibuni serikali ya awamu ya tano ya Tanzania imefanya jitihada mbalimbali za kuongeza ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam. Jitihada hizo zimeibua kashfa mbalimbali zilizohusisha upotevu wa makontena kutoka bandari ya Dar-Es-Salaam na  bandari kavu (ICD) na kusimamishwa kwa muda kwa kampuni zaidi ya mia (100) za uwakala wa mizigo bandarini (Clearing and Forwarding). Habari hizi zimesababisha wafanyabiashara wa nje ya Tanzania kuhofia usalama wa mizigo yao ikipitishwa bandari ya Dar es Salaam na hivyo kuchagua kupitishia bandari nyingine wanazohisi zina usalama zaidi.

TATOA imeisha wasiliana na Serikali kuhusu vizingiti hivi vya biashara. Imepeleka andiko kwa Waziri Mkuu ; Waziri wa Fedha na Waziri wa Uchukuzi ikipendekeza hatua mbalimbali za kuchukua kusuluhisha matatiza haya ikiwemo kuondolewa kwa kodi na mifumo kandamizi inayoongeza gharama za kupitishia mizigo bandari ya Dar es Salaam.

TATOA pia imeomba na kukubaliwa kukutana na Kamishna Mkuu wa TRA Jumatatu tarehe 11 April saa 9 mchana kujadili matatizo haya. Wanachama watajulishwa matokeo ya juhudi zetu.

No Comments

Post a Comment