Mkataba wa ujenzi wa Bandari Kavu, Ruvu wasainiwa

Tarehe 14 Februari 2017, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ilisaini mkataba na kampuni ya SUMA JKT ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa ajili ya ujenzi wa Bandari Kavu (ICD) yenye ukubwa wa hekta 500 Ruvu mkoani Pwani. Mrradi unaotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao unatarajiwa kuchukua wiki 9 kukamilika kwa gharama ya shilingi za Kitanzania Bilioni 7.3.

Akizungumza katika hafla ya kutia saini mkataba huo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Kazi, Ujenzi, na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa alieleza matumaini ya serikali kwamba ICD itasaidia kupunguza msongamano wa magari katika Bandari ya Dar es Salaam na katika mji wa Dar es Salaam kwa ujumla kutokana na makontena yatasafirishwa kutoka bandarini hadi katika ICD hiyo ya Ruvu kwa treni na wenye malori kutumika kuisafirisha kwenda katika mikoa na nchi za jirani. Prof Mbarawa alisema mpango wa serikali ni kuhamisha ICDs zote kwenda nje ya jiji la Dar es Salaam katika siku zijazo.

Prof Mbarawa pia alibainisha kuwa kuna mipango inaendelea, kujenga gati mpya mahsusi kwa ajili ya magari pamoja na kupanua gati moja hadi saba katika bandari ya Dar es Salaam. Wakandarasi kwa ajili ya miradi hiyo wameshatafutwa, kinachoendelea sasa hivi ni mikataba imepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya mapitio na shughuli ya kusaini makubaliano itafanyika ndani ya mwezi mmoja.

Hivi sasa, meli kubwa hushindwa kutia nanga bandari wakati maji yakipungua lakini upanuzi wa bandari unaotaka kufanyika utaruhusu meli kutia nanga wakati wowote, Waziri Mbarawa alifafanuai.

No Comments

Post a Comment